Font size:
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Dotto Biteko, ameuagiza Wakala wa Umeme Vijijni (REA), kupanya tathimini ya wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme na kuachana na wale wanaoshindwa kuendana na kasi ili ifikapo Juni 2024, miradi yote nchini iwe imekamilika.
Ametoa agizo hilo leo, Nov. 15, 2023, mkoani Mtwara, wakati akiwasha umeme katika vijiji vya Nachenjele na Naliendele katika ziara yake ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kwamba serikali imetoa Bilioni 170 kwa ajili ya utelekezaji wa miradi ya REA, mkoani humo.
Dkt. Biteko ameitaka REA na TANESCO kutumia vifaa vya usambazaji umeme vinavyozalishwa na viwanda vya ndani, badala ya kuagiza nje ya nchi na kwamba katika kukuza viwanda vya ndani, REA na TANESCO wanapaswa kuhakikisha wanaatumia bidhaa zinazozalishwa na viwanda hivyo ili kuchochea ukuaji wa uchumi na upatikanaji wa ajira kwa wananchi.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugezi Mkuu wa REA, ambaye ni Mkurugenzi wa Umeme Vijijini, Mhandisi Jones Olotu, amesema tayari wamesambaza umeme katika vijiji 384 kati ya 785 ambapo vilivyosalia viko katika utekelezaji.