Mvua za El Nino husababishwa na mabadiliko katika joto la bahari la Pasifiki Mashariki. Kawaida, upepo huvuma kutoka mashariki kwenda magharibi juu ya eneo hilo la bahari, na hii husababisha maji yenye joto kujilimbikiza upande wa magharibi wa Pasifiki.
Wakati wa El Nino, hali hii hubadilika: upepo hupungua au kubadilika mwelekeo, na maji yenye joto yaliyojilimbikiza magharibi huanza kusambaa kwenda mashariki. Hii husababisha maji baridi ya chini ya bahari kuja juu na kusababisha mabadiliko ya hali ya hewa duniani.
Wataalamu wa hali ya hewa wanasema kwa kawaida, El Nino huleta mvua nyingi na hali ya hewa ya joto katika maeneo ambayo kwa kawaida ni makame, na inaweza kusababisha mafuriko na athari nyingine za hali ya hewa.
Shirika la Hali ya Hewa Ulimwenguni (WMO), linasema El Nino hutokea kwa wastani kila baada ya miaka miwili hadi saba, na vipindi vya kawaida vya mvua hii mara nyingi huchukua miezi tisa hadi 12.
Nalo Shirika la Afya Duniani (WHO), linasema athari ambazo huambatana na mvua hizo ni maradhi, upungufu katika uzalishaji wa chakula hivyo kuongezeka kwa bei ya vyakula na mafuriko.
Katika Msimu huu wa Vuli, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imetabiri uwepo wa mvua za El Nino katika maeneo yote yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka.