Taarifa njema ni kwamba, uwakilishi wa Bara la Afrika kufuzu moja kwa moja Kombe la Dunia umeongezwa kutoka timu tano hadi tisa kwenye Kombe la Dunia la 2026 baada ya FIFA kupanua washiriki hadi timu 48.
Hatua hiyo imetoa motisha ya ziada katika safari ya kufuzu, ambayo itaendelea hadi Oktoba 2025, huku nafasi hizo tisa za kufuzu moja kwa moja zinatarajiwa kuwa na ushindano mkali kati ya timu za bara la Afrika.
Kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania “Taifa Stars” tayari kimeanza safari ya kuelekea Morocco kuchuana na Niger mechi ya kundi E kufuzu Kombe la Dunia.
Mchezo huo umeratibiwa kuchezwa katika uwanja wa Marrakech Grand, ulioko mjini Marrakech, siku ya Jumamosi, Novemba 18, mwaka huu.
Kwa upande wao Uganda, itakutana na Guinea Ijumaa, Novemba 17, 2023 katika uwanja wa Stade De Municipal mjini Berkene, kabla ya kumenyana na Somalia, katika uwanja huo huo siku nne baadaye zikiwa ni mechi za Kundi G.
Harambee Stars, timu ya taifa ya Kenya, yenyewe iliondoka Jumatano wiki hii, kuelekea Gabon tayari kukabiliana na Gabon katika mechi yake ya ufunguzi ya kufuzu, kundi F, Alhamisi, Novemba 16, 2023.
Mapema wiki hii, makocha wote wa timu zote za Kenya, Uganda na Tanzania wamevitaja vikosi vyao tayari kwa safari hiyo ya kufuzu Kombe la Dunia 2026.
Jijini Dar es Salaam, Tanzania, timu ya taifa ya Soka ya Burundi nayo inachuana na The Gambia leo Alasiri, mechi ya kufuzu (Kundi F).
Imeandaliwa na William Shechambo, kwa msaada wa Intaneti.