OFISI ZA UDART JANGWANI ZIHAMISHWE

Font size:

Bwana atakufanya kuwa kichwa, wala si mkia; nawe utakuwa juu tu, wala huwi chini; kuyaangalia na kufanya” Kum 28:13. Kuna mambo ambayo kama tunataka kupiga hatua kiuchumi, kisiasa, kijamii na kiutamaduni lazima Serikali ijiepushe na kuchukua maamuzi ya kisiasa, au hata maamuzi ya kuwafurahisha wawekezaji! Kuna maswali yanayokosa majibu ukijiuliza kigezo kilichotumika maegesho ya magari yaendayo kasi kuwa jangwani!

Hadi sasa ofisi za UDART ziko jangwani wilaya ya Ilala, sijajua kama mabasi haya yamekatiwa bima ya aina gani? Na hata kama yamekatiwa bima hakuna nchi yeyote hapa duniani inayoweza kukubali kujiweka rehani kuruhusu janga kama hili kuukuta mradi wa mabilioni ya fedha za wananchi kuteketea kwa uamuzi ambao unaweza kuepukwa.

Achilia mbali mabasi ya UDART kuna habari ambazo zinasambaa kuwa upo mpango wa kujengwa daraja refu kutoka Ofisi za Zimamoto pale Fire hadi Magomeni, hizi ni habari njema kama zipo na kama zitafanyiwa kazi! Watu wanateseka sana kipindi cha mvua. Toka habari zimetolewa yapo madaraja makubwa ambayo yamekwisha kujengwa! Madaraja hayo ni lile la Mto wami, na hili ambalo sasa linaendelea kujengwa kule Mwanza. Kwa picha hii inaonyesha kuwa tunao uwezo mkubwa kukamilisha miradi yetu ya ndani kwa kutumia pesa zetu za ndani.

Katika Makala zilizopita tumeuzungumzia sana mradi huu, hata kufikia wasomaji wengi kutoa maoni yao, Makala ile aione Waziri wa Uchukuzi! Kama huu ni mradi mmoja ambao unatutia mashaka, je kuna miradi mingapi yenye dosari, tena ambayo imetumia pesa nyingi za wananchi! Inawezekana wataalamu wetu wana hoja lakini wameamua kukaa kimya na kuwaachia wanasiasa! Lakini hiyo sio sawa inatupasa tuamke sasa, tena tufanya uamuzi wa makusudi kabisa, maeneo yanayohusu utaalamu waachiwe wataalamu!

Akizungumza leo Machi 16 Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Udart,  Deus Bugaywa amesema wamehamisha ofisi hizo ili shughuli zinazofanywa na mradi huo zisiweze kutetereka kutokana na mvua zinazoendelea.

Tuangalie eneo la makazi ya watu! Hatujachelewa bado, sasa hivi ujenzi unaoendelea maeneo ya Kariakoo nikichukulia mfano wa mji wa Dar es Salaam, majengo yanayojengwa ni ya magorofa, nay ale ya kwenda chini, na hii ni kutokana na kugundua kuwa kuna uhaba mkubwa wa ardhi sasa hivi!

Ujenzi wa majengo yaliyojengwa Magomeni unaweza kufanyika pia Ilala, hasa zilipo nyumba za Serikali, swali je haiwezekani kujenga majengo ya aina hii, na kuweka muonekano wa jiji kuwa wa kupendeza! Baba wa Taifa aliwahi kusema kupanga ni kuchagua, tunaweza kabisa kubadilisha muonekano wetu kwa kufanya mageuzi sisi wenyewe, ni hakika kuishi katika maisha duni ni kujitakia sisi wenyewe!

Kuwa na barabara mbovu ni kujitakia, na ni mambo yanayofanyika kwa makusudi kabisa, haiwezekana kutengeneza barabara ya lami ikadumu kwa miezi michache, kisha inaombewa tena pesa, huu ni mchezo hatarishi! Kama kweli tunataka maendeleo tuache kabisa kuchekeana na watu ambao hawaitakii mema nchi yetu! Huduma za jamii zisifanyiwe mzaha.

Serikali itamke wazi maeneo ya jangwani, na maeneo yanayofanana na hali za namna hiyo hayafai kwa ujenzi wa aina yeyote ile! Yapo mambo mengi hasa katika jiji hili la kibiashara ambayo yanaweza kuboreshwa! Mfano usafiri wa treni.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila alipofanya ziara ya ghafla kukagua usafiri wa treni amejionea mambo ambayo yamemchanganya sana. Inakuwaje TRC, baada ya ubunifu wa aliyekuwa Waziri Mhe Mwakyembe, hadi treni ikaitwa ya Mwakyembe wameshindwaje kujiongeza na kuiboresha huduma ya treni! Ikiwa kila siku wanaingiza pesa inakuwaje waendelee kutumia mabehewa makuukuu! Kuna changamoto ya usafiri inayowakabili wakazi wa Gongo la mboto na maeneo jirani, inashindikana nini kuongeza safari za treni ili kukabiliana na adha hiyo.

 

Kama inafikia wakazi wa Dar es Salaam ambao wametoka katika shughuli za ujenzi wa taifa , wamechoka haiwezekani kupata usafiri ambao wataufurahia basi kuna haja ya kujua haya mateso yana makusudi gani! Tufikie wakati mtu aliyeko katika taasisi akiripotiwa kuwa na kauli mbaya kwa mteja asiachwe hivi hivi awajibishwe.

Serikali inatumia mabilioni ya pesa, kuhakikisha jamii inahudumiwa vema kwa nini mtu mmoja awe kikwazo? Nimezungumza kuhusu mazingira mazuri ya kuweka makazi ya ofisi za umma yote kwa yote juhudi zinazofanywa ujenzi wa barabara za mwendokasi utasaidia wakazi wa maeneo ya nje ya mji kama vile Gongo la Mboto, Chanika, Chamazi, Kibaha, na kwingineko watanufaika pia. Hata hii mipango ya baadaye kujenga barabara za mwendokasi kutoka Maktaba hadi Ohio, Ohio-Morocco na Morocco -Tegeta sawa na Kilometa 30.1, hata ule mpango wa kujenga barabara ya Sam Nujoma na upanuzi wa barabara ya Kimara, unafaa sana.

Wananchi tufahamu kuwa Serikali inatumia fedha kutoka Benki ya Dunia, IMF na nyingine, na zile  zinazotokana na vyanzo vya ndani vya mapato, lazima zitumike kwa umakini na uangarifu mkubwa. Ona barabara ya Gerezani- Mbagala yenye urefu wa Kilometa 20.3, inavyopendeza, nayo imegharimu mabilioni ya pesa. Mungu atusaidie kujali vitu vya kwetu, hebu na tuwe wabunifu, tusingoje kusukumwa katika kufanya kazi.

Mwandishi ni Mchg. Christosila Kalata - christosiler@yahoo.com  0713 29 86 86.

or

For faster login or register use your social account.

Connect with Facebook