Siku chache baada ya Mkoa wa Morogoro kuripotiwa kukumbwa na mvua kubwa iliyosababisha vifo vya watu watano na majeruhi zaidi ya 200, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imeutaja tena mkoa huo na mingine saba, kuwa katika picha za rada ikioneshwa kukumbwa na mvua kubwa kwa siku tano mfululizo kuanzia leo Januari 30, 2024.
Kwa mujibu wa TMA, mikoa hiyo ni Morogoro, Lindi, Iringa, Mtwara, Mbeya, Songwe, Njombe na Ruvuma ambapo inatarajiwa kupata mvua za juu ya wastani wake wa kawaida.
Imesema athari zinazoweza kutokea kufuatia hali hiyo ni uharibifu wa miundombinu na makazi ikiwemo nyumba kuzungukwa na maji pamoja na athari za baadhi ya shughuli za kiuchumi.
TMA imewataka wananchi wa maeneo hayo kuchukua tahadhari na kujiandaa na dharura zinazoweza kujitokeza.