Mkuu wa KKKT, Askofu Dkt. Alex Gehaz Malasusa, ameongoza mamia ya waombolezaji kuaga mwili wa aliyekuwa Waziri Mkuu mstaafu Hayati Edward Lowassa, katika ibada iliyofanyika Kanisa Kuu la KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Azania Front.
Akihubiri katika Ibada hiyo, Askofu Dkt. Malasusa aliwakumbusha Wakristo na waombolezaji kwa ujumla kutafuta uso wa Mungu na kusogea mbele zake kwa ibada ya shukrani na maombi, hususani nyakati za huzuni, ili Mungu afanyike faraja ya kweli kwao na kuwaganga mioyo wale wote wenye huzuni.
Aliongeza kwa kuwasihi Wachungaji kutoleta Kanisani, miili ya watu wasiopenda ibada ambao enzi za uhai wao waliishi bila kufanya ibada kwani kwa kufanya hivyo wanaikosea miili hiyo, huku akisisitiza familia ya Hayati Lowassa, kuendelea kuwa na moyo wa kupenda Ibada.
Baadhi ya waombolezaji, akiwemo Mchungaji wa KKKT- DMP Dkt. Eliona Kimaro, walisema mchango wa Hayati Lowassa katika kuimarisha elimu nchini hautasahaulika, kwa sababu alitoa mchango mkubwa katika uanzishaji wa shule za kata.
Wakitoa salamu za rambirambi baadhi ya viongozi wastaafu wa serikali akiwemo Rita Mlaki, walisema Hayati Lowassa alikuwa mtu aliyependa uwazi na hakupenda kubeba jambo moyoni.
“Lowassa alikueleza ukweli pale inapobidi lakini kubwa zaidi alimpenda Mungu na alifunga kila Kwaresma ilipoanza,” alisema Rita.
Mbunge mstaafu wa viti maalumu Ruth Mollel, naye alisema Lowassa alikuwa kiongozi jasiri mwenye kusimamia misimamo yake na aliyejaliwa hekima ya ukimya hata kama alikuwa anapitia changamoto iliyombidi azungumze alichagua kuwa kimya.
Mwenyekiti wa Bodi, Upendo Media, Theophil Mlaki, alisema Edward Lowassa alikuwa na mchango mkubwa katika mchakato wa kuanzisha Upendo TV na Upendo Redio na daima wataendelea kumkumbuka na kumuombea.
Naye mjumbe wa bodi hiyo, Jesse Kwayu, alieleza kwa kina, namna Lowassa alivyokuwa muwajibikaji na kuleta nidhamu katika utumishi wa Umma.
Mwili wa Hayati Edward Lowassa, uliagwa Alhamisi, Usharika wa Azania Front na kusafirishwa kuelekea mkoani Arusha Ijumaa na jana ulizikwa wilayani Monduli, maziko yaliyohudhuriwa pia na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.