Hamas yaachia huru raia wawili wa Marekani

Font size:

Kundi la wanamgambo la Hamas limetangaza kuwaachia huru Wamarekani wawili ambao ni miongoni mwa mateka inaowashikilia, ikitaja "sababu za kibinadamu" pamoja na kutuma ujumbe kwa rais Joe Biden ambaye kwa ameunga mkono kwa dhati Israel katika vita vyake dhidi ya kundi hilo.

Msemaji wa tawi la kijeshi la Hamas Abu Ubaida ametoa taarifa ya kuachiwa kwa mateka wawili, ikiwa ni mara ya kwanza tangu wanamgambo wa kundi hilo walipoishambilia Israel Oktoba 7 na kuwaua watu 1,400 wengi wao wakiwa ni raia na kuwachukua watu wengine karibu 200 kama mateka. Kwenye taarifa yake hiyo Abu Ubaida amesema mateka hao wameachiwa huru kutokana na juhudi za upatanishi za Qatar.
 

Ofisi ya waziri mkuu wa Israel imethibitisha taarifa za kuachiliwa mateka hao wawili jana usiku. Afisa wa Israel ambaye anashughulikia masuala ya mateka na watu waliopotea Brigedia Jenerali Gal Hirsch, amewapokea mateka hao katika mpaka wa Ukanda wa Gaza huku taarifa zaidi zikisema kwamba wanawake hao wawili walikuwa njiani kuelekea katika kambi ya kijeshi kuungana na familia zao. Daniel Hagari ni msemaji wa jeshi la Israel IDF na ameeleza kwamba, "Judith Tai Raanan na Natalie Shoshana Raanan, mama na binti, wameachiliwa kutoka kwa kundi la kigaidi la Hamas jioni hii, na sasa wako mikononi mwa askari wa IDF na vikosi vya usalama katika eneo la taifa la Israeli."

Hapo awali, jeshi la Israel lilisema kwamba watu wengi wanaoshikiliwa mateka bado wako hai.

Hayo yakiarifiwa, Israel imeyaonya makundi ya misaada ya kiutu yaliyoko Ukanda wa Gaza kuwaondoa watu katika hospitali kubwa na shule tano kutokana na kuwepo uwezekano wa shambulio kubwa. Hospitali ya Al-Quds iliyoko kaskazini mwa Gaza, imekabiliwa na mashambulizi makali ya anga ya Israeli tangu Hamas ilipofanya mashambulizi yao makubwa zaidi kuwahi kutokea dhidi ya Israeli mnamo Oktoba 7.

or

For faster login or register use your social account.

Connect with Facebook