PAPA LEO XIV - RAIA WA KWANZA WA MAREKANI KUONGOZA KANISA KATOLIKI DUNIANI

Font size:

CHINI ya saa 48 za kujitenga kwa makardinali 133 wa Kanisa Katoliki Duniani katika mji wa Vatican, ili kumpata mrithi wa Papa Francis, jukumu hilo walilikamilisha kwa kumchagua Kardinali Robert Prevost kuwa Papa Leo XIV.

Prevost, ambaye ni mzaliwa wa Chicago, Marekani, anakuwa Papa wa kwanza kutoka Marekani katika historia ya Kanisa katoliki. Pia ni raia wa Peru, ambako alihudumu kama Mmisionari kwa miaka mingi.

Kabla ya kuchaguliwa kuwa Papa, Prevost alikuwa mkuu wa idara ya maaskofu katika Kanisa katoliki, akisimamia uteuzi wa maaskofu wapya.

Ingawa anachukuliwa kama kiongozi wa kati kwa msimamo wake, amekuwa mstari wa mbele katika kuunga mkono makundi yaliyotengwa, akiiga mfano wa mtangulizi wake Papa Francis.

Prevost alizaliwa Septemba 14, 1955 na kusomea theolojia katika Chuo cha Catholic Theological Union, Chicago.

Alipokuwa na umri wa miaka 27, alitumwa Roma kwa masomo ya upadre na kupewa daraja la upadri mwaka 1982.

Baadaye alikwenda Peru ambako aliongoza seminari ya Waaugustino mjini Trujillo na kisha kuwa msimamizi wa kitume wa dayosisi ya Chiclayo mwaka 2014.

Mwaka mmoja baadaye aliteuliwa kuwa Askofu na mwaka 2023, Papa Francis alimteua kuwa Kardinali.

Kwa utaratibu wa Kanisa Katoliki, mara baada ya kuchaguliwa Papa mpya, hupewa nafasi ya kuchagua jina jipya ili kuashiria mwanzo mpya wa utumishi wake kama kiongozi wa Kanisa katoliki.

Desturi hii ilianza na Mtume Petro, ambaye jina lake la kuzaliwa lilikuwa Simon ambapo Papa mpya huashiria malengo na maono yake ya uongozi.

Papa Leo XIV alichagua jina hilo kwa sababu maalumu. Kwa mfano, Papa Francis alichukua jina hilo akimuenzi Mtakatifu Francis wa Assisi, aliyefahamika kwa kujitolea kusaidia watu masikini na kuijenga upya imani ya Kanisa.

Kwa kuchagua jina la Leo, Prevost anaweza kuwa ameashiria dhamira ya kuendeleza mafundisho ya watangulizi wake au kuleta mwelekeo mpya wa uongozi.

or

For faster login or register use your social account.

Connect with Facebook