MILA POTOFU CHAKA LINALOCHANGIA NDOA ZA UTOTONI

Font size:

WAKATI kumekuwa na juhudi nyingi nchini zinazolenga kukomesha ndoa za utotoni, jamii mbalimbali kuendelea kukumbatia mila na tamaduni potofu ni miongioni mwa mambo yanayoelezwa kuwa vikwazo vya kufanikisha harakati hizo.

Ukweli huu unathibitishwa na Chifu Mkuu wa kabila la Wamwera, Nakotyo Malibiche wa IV, ambaye anasimamia jamii yote ya kabila hilo mkoa wa Lindi, ambaye anasema mila na tamaduni zimekuwa sababu kubwa kwa makabila mengi kuendelea na utaratibu wa ndoa utotoni.

Akizungumza na gazeti hili wilayani Nachingwea, Chifu Nakotyo anasema mkoani Lindi tatizo la ndoa za utotoni lipo kwa makabila mengine yanayohamia ambayo si wenyeji wa mkoa huo, ambao kwa asili si watu wa kabila la Wamwera, analoliongoza.

“Kwa kweli hili tatizo lipo kwenye jamii nyingi, Wamwera tumejitahidi sana kudhibiti kwa sababu tumepeana taarifa kuhusu umuhimu wa elimu kwa watoto wote bila ubaguzi, hivyo ni nadra sana kusikia ndoa ya mtoto kwa Wamwera.

“Katika maeneo yetu kuna wahamiaji kutoka kanda ya Ziwa, kabila la Wasukuma ambao ni wafugaji na Wamakonde kutoka mkoa jirani wa Mtwara, hawa wote wana mila fulani ambazo zinawaruhusu wao kushiriki ndoa za utotoni, ili kuongeza uzao katika ukoo,” anasema.

Chifu Nakotyo anasema mila hizo potofu zinafifisha na kuzima ndoto za watoto wengi kwa kuwaingiza katika ndoa wakiwa bado na umri mdogo. Anatoa rai kwa viongozi wengine wa kimila kuwa mabalozi wa kukemea kwa nguvu zote ndoa za utotoni.

Pia anasema katika jamii nyingi nchini kwa sasa kuna malezi mabovu ya watoto hali inayozalisha vijana wengi wenye tabia mbaya kama kukosa usikivu kiasi cha kutowatii hata wazazi wao. Tabia hizo zisizokubalika katika jamii ni pamoja na baadhi ya watoto kukataa kwenda shule, hali hiyo mara nyingine huwasukua wazazi katika jamii mbalimbali kuamua kuwaozesha ili kuambulia chochote kitu kama mahari.

Mkuu wa Jimbo KKKT Nachingwea

Mchungaji Kiongozi wa KKKT Usharika wa Nachingwea, Kastory Magulu, ambaye pia ni Mkuu wa Jimbo la Nachingwea, anasema tatizo la ndoa za utotoni husababisha ukatili wa kijinsia, ukosefu wa elimu, utegemezi wa kiuchumi na madhara ya kiafya kwa wasichana.

“Biblia inatuagiza kumlea mtoto katika njia impasayo ikiwamo kuhakikisha anapata haki zake katika nyanja zote ikiwamo elimu. Unapomuoza katika umri mdogo ni kumnyima haki yake ya msingi,” anasema.

Anasema viongozi wa dini, mashirika na serikali wanapendekeza mabadiliko ya sheria ya ndoa inayoendelea kutekelezwa hapa nchini na kuimarisha elimu na uhamasishaji wa jamii kukomesha tatizo la ndoa za utotoni.

“Ndoa ni maagano ya watu wawili waliokomaa kimwili na kiakili na si vinginevyo. Ndoa ina wajibu wake, misingi na haki zake inamtaka mtu awe na ukomavu wa kiakili na kiimani pia, unapomlazimisha msichana kuingia kwenye ndoa za utotoni unapingana na uhalisia,” anasema.

Mchungaji huyo aliongeza: “Kumuoza binti ambaye hajakomaa kiakili, kimwili na kifikra ni kupingana na matakwa na mapenzi ya Mungu na kupingana na uhalisia.

“Unapomlazimisha mtoto kuingia katika ndoa anakosa elimu na kuingizwa kwenye makubaliano ambayo kwa akili na ukomavu wake hana uelewa wa kutosha.

“Hivyo atapata watoto wakati uwezo wake wa kuwa mama au baba hautoshi, ni vema wakaachwa hadi wawe wakomavu, kimwili, kiakili na kihisia ili kupokea majukumu hayo kikamilifu.”

Mkuu huyo wa jimbo anasisitiza kuwa: “Hapa Nachingwea, kila Jumapili ya mwisho wa mwezi neno la Mungu pamoja na mwongozo wa Kalenda ya Kanisa, lazima tufundishe kuhusu kuheshimu utu na kukemea ukatili ukiwemo huu wa ndoa za utotoni na mimba katika umri mdogo.”

Msimamo wa Kanisa

Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), kupitia Mradi wake wa ‘Hakuna marefu yasiyo na mwisho’ limejizatiti katika kuhakikisha ndoa za utotoni zimefika mwisho.

Mradi huo una lengo la kuwezesha mabadiliko chanya ya mila na desturi kandamizi, kuwatetea wasichana walio katika mazingira hatarishi kwa kuchagiza mabadiliko ya sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 ambayo inaruhusu kuolewa kwa watoto, ilihali Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 inaweka bayana kwamba mtoto ni lazima wawe chini ya uangalizi wa wazazi au walezi mpaka wanapofika umri wa miaka 18.

Sheria hizi mbili zinagongana na hukumu mbili, ya Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa ya Tanzania katika kesi maarufu ya Rebeca Gyumi dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Tafiti mbalimbali nchini zimebainisha kuwa ndoa za utotoni zimekuwa zikiendelea chini ya viongozi wa kimila na kupewa baraka na baadhi ya viongozi bila tatizo lolote.

Mathalani, utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria Tanzania (TDHS-MIS) mwaka 2022, ulionyesha kuwa asilimia 20.3 ya Watanzania wenye miaka 15-19 wameolewa, wanaishi pamoja au walikwisha kuwa kwenye mahusiano na wametengana. Kati ya walioolewa wa umri huo asilimia 30.6 walikuwa na ndoa zilizosajiliwa na kuwa wana vyeti.

Vilevile, takwimu hizo zinaonyesha wanawake wenye miaka 25-49 waliolewa wakiwa na wastani wa miaka 19.8. Utafiti unaonyesha kuwapo kwa uhusiano wa moja kwa moja kati ya kiwango cha elimu na ndoa za utotoni. Katika ripoti hiyo wanawake wasio na elimu waliolewa wakiwa na wastani wa umri wa miaka 18.1 ikilinganishwa wastani wa umri wa miaka 23.7 kwa waliokuwa wamehitimu elimu ya sekondari au elimu ya juu.

UNICEF yatia neno

Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Watoto (UNICEF), linaeleza kuwa mkataba wa Kimataifa wa Haki ya Mtoto unafafanua kuwa: “Mtoto ni binadamu yeyote ambaye kiumri yuko chini ya miaka 18 isipokuwa pale ambapo sheria imetamka vinginevyo.”

Hata hivyo, UNICEF licha ya kuwapo kwa mikataba hiyo na sheria nyingine zinazofafanua haki za watoto, bado jamii nyingi duniani na nchini zinaendeleza kubariki ndoa za utotoni.

Tafiti hizi zimethibitisha kwamba ndoa za utotoni husababisha matatizo makubwa hasa kkwa watoto wa kike ikiwamo unyanyasaji wa kijinsia, kunyima haki ya masomo na kukosa fursa za kujiendeleza kiuchumi.

Aidha, UNICEF wanasema kuwa wasichana wadogo wanapopata ujauzito, wanakuwa katika hatari kubwa ya kupoteza maisha wakati wa kujifungua, ikilinganishwa na wale wenye umri wa kuanzia miaka 20 na kuendelea. Shirika hili linaeleza kuwa, hata mabinti hao wakipona, watoto wao wapo kwenye hatari ya kupoteza maisha wakati wa kujifungua au miezi michache baadaye.

Takwimu za UNICEF za mwaka 2024 zinaeleza kuwa asilimia 21 ya wanawake vijana duniani walikuwa wameolewa kabla ya kufikia umri wa miaka 18, hii inamaanisha kuwa, wanawake milioni 650 walikuwa wameolewa wangali watoto. Tathmini ya takwimu hizo zinaonyesha kuwa kwa mwaka watoto milioni 12 huolewa kila mwaka.

Ndoa za utotoni nyingi zinaelezwa kuwa zaidi barani Afrika eneo la kusini mwa Jangwa la Sahara likibeba asilimia 37 ya ndoa hizi.

or

For faster login or register use your social account.

Connect with Facebook