NA WILLIAM SHECHAMBO
Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), inaadhimisha Siku ya CCT ambayo ni maalumu katika kudumisha Umoja wa CCT na kuitegemeza jumuiya hiyo katika utoaji wa huduma za kitume na kijamii miongoni mwa wanachama wake.
Ibada ya maadhimisho hayo inafanyika leo, katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Mashariki Ziwa Victoria (DMZV), Usharika wa Ebenezer Pasiansi, jijini Mwanza.
Akizungumza hivi karibuni, Godlisten Moshi, ambaye ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa CCT, alisema, Ibada ya maadhimisho ya CCT Day itaambatana na sadaka maalumu ya utume kwa wahitaji kiroho na kimwili.
Wakati maadhimisho hayo yanafanyika, jumuiya hiyo imejinasibu kuwa mstari wa mbele katika kuhubiri haki, umoja wa kitaifa, amani ya nchi, demokrasia na utawala bora.
Katika taarifa yake ya utendaji kwa mwaka 2024/2025, CCT imeeleza kuwa hayo ni masuala mtambuka na muhimu katika ustawi wa nchi pia ni nguzo ya utaifa.
Pia imeeleza kuwa, katika kipindi cha hivi karibuni, hali ya amani, utunzwaji wa haki za binadamu, demokrasia na utawala bora nchini, imeendelea kupata dosari.
“Mfano wa dosari hizo ni pamoja na wapinzani kuendelea kubanwa na kunyimwa haki zao za kikatiba na kidemokrasia, mathalani polisi kuwazuia wasifanye maandamano kupinga mambo ambayo wanaona hayaendi sawa...,” imeeleza taarifa hiyo ya CCT.
Kuhusu uchaguzi mkuu
Vilevile jumuiya hiyo imesema, imeendelea kushiriki katika mchakato wa uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025, kwa kutoa elimu ya uraia, elimu ya uchaguzi kwa viongozi wa CCT na kwa Watanzania wote kwenye baadhi ya maeneo nchini.
“CCT imeendelea kuhamasisha Watanzania wote ama kujiandikisha katika Daftari la kudumu la mpiga kura au kuhuisha taarifa zao katika daftari hilo, pamoja kushiriki kupiga kura kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 ili kuwapata viongozi bora watakao ongoza nchi yetu kwenye nafasi za udiwani, ubunge na urais,” imesisitiza.
Pia imeongeza, CCT itaendelea kuisihi Tume Huru ya Uchaguzi na Mamlaka zote zinazoratibu na kusimamia uchaguzi kuondoa dosari zote zinazoonekana katika michakato ya chaguzi mbalimbali nchini.
Vitendo vya watu kutekwa
Taarifa ya CCT imeeleza kuwa, kupitia vyombo vya habari, imeendelea kusikia na kusikitishwa na vitendo vya kikatili vya upotevu wa watoto na watu wazima maeneo mbalimbali nchini hadi kusababisha kuzua taharuki kubwa nchini.
“Vyombo vya habari vimeendelea kutoa taarifa za matukio ya kupotea kwa watu ambao wakati mwingine hupatikana wakiwa wamefanyiwa ukatili mkubwa pamoja au kuuwawa.
“Tunaendelea kuisihi serikali kufuatilia kwa kina na kufanya uchunguzi dhidi ya taarifa hizo na kuchukua hatua kali za kisheria ili kudhibiti matukio hayo makubwa na ya kihalifu yasiendelee kutokea nchini.
“Viongozi wa CCT wamekuwa wakiisihi Serikali kuzifanyia kazi taarifa za kupotea au kutekwa watu bila kuzipuuza au kuzikanusha,” imesisitiza CCT katika taarifa hiyo.
Vyama vya siasa na dremokrasia
Katika eneo la ushiriki wa vyama vya siasa kwenye michakato ya demokrasia, CCT imebainisha kuwa ni haki ya msingi ambayo ipo kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano Tanzania kuruhusu vyama vya siasa kufanya shughuli zao za kisiasa kwa kadiri ya matakwa ya sheria za nchi.
Hata hivyo, imesema imeendelea kushuhudia watu wakikamatwa, kupigwa, kuwekwa kizuizini na jeshi la polisi na kufunguliwa kesi kwa sababu za kisiasa, hasa pale wanapoonekana kukosoa baadhi ya kanuni na sheria zenye utata za uchaguzi.
“CCT inalaani matukio yaliyojitokeza hivi karibuni ya uvunjifu mkubwa wa haki za binadamu, ukiukwaji wa misingi ya utawala bora na uvunjifu wa amani na utulivu.
“Matukio haya ni pamoja jeshi la polisi kutumia nguvu kubwa kuwatawanya kwa kuwapiga na kuwaumiza sana baadhi ya wafuasi wa CHADEMA waliojitokeza kwenda mahakamani kusikiliza kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wao Tundu Lisu Aprili 24, 2025.
“Pia kushambuliwa na kujeruhiwa kwa kiongozi wa kidini Padri Charles Kitima, ambaye ni Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu wa Kikatoliki nchini (TEC), na kutekwa pamoja na kupotea kwa watu mbalimbali mfano; mwanaharakati Faluka Nyagali (Mdude), kuuawa kwa mwanachama wa CCM Mwanza na mengine kama hayo,” imebainisha CCT katika taarifa hiyo.
Jumuiya hiyo inayoongozwa na Mwenyekiti wake Askofu Dkt. Fredrick Shoo wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini, inajumuisha Makanisa ya kiprotestanti 12 na vyama vya kimitume 14 kutoka maeneo yote nchini na jukumu lake kuu ni kufanya huduma ya kumhudumia mwanadamu kiroho na kimwili.