NA MWANDISHI WETU
ASKOFU Dkt.
Alex Gehaz Malasusa, amesema Dayosisi ya Mashariki na Pwani imepewa heshima ya
kuwa mwenyeji wa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Kiinjili wa Kimisioni (UEM), kwa
niaba ya wanachama wa umoja huo bara la Afrika kuanzia Septemba 14 hadi 19,
mwaka huu, Dar es Salaam.
Katika
taarifa yake kwa wanahabari, Askofu Dkt. Malasusa ameeleza kuwa, Washarika wote
wanaalikwa katika Ibada ya ufunguzi rasmi wa Mkutano huo, itakaofanyika
Usharika wa Mbezi Beach, Jumapili ya Septemba 14 kuanzia saa 7.00 mchana.
“Wapendwa watu wa Mungu UEM inatokana na kazi ya Misheni ya Rhenish, Misheni ya Betheli na Misheni ya Zaire. Washiriki wa UEM leo ni makanisa ya Kiprotestanti Barani Afrika, Asia na Ujerumani, ambayo yamekuwa yakifanya kazi pamoja kwa usawa tangu 1996.
“Wanachama wa UEM wako Ujerumani, Asia (Indonesia, Ufilipino, Hong Kong na Sri Lanka) na Afrika ni nchi za Botswana, Namibia, Afrika Kusini, Cameroon, DRC, Rwanda na Tanzania,” alisema Askofu Malasusa.
Alisisitiza
kuwa, UEM inatafsiri uelewa wake katika maeneo matano ambayo ni Maendeleo,
Uinjilisti, Utetezi, Diakonia na Udugu (Partnership) na kuongeza kuwa, katika
siku ya ufunguzi Kanisa limewaalika viongozi wa serikali na taasisi za serikali
na mabalozi wote kutoka katika nchi wanachama wa UEM na wadau wote wa CCT na vyama
vya kiinjili nje na ndani ya nchi.
Kaulimbiu
ya Mkutano Mkuu wa UEM wa 2025 ni: “Boriti Katika Jicho Letu” Ubaguzi katika Kanisa na Udiakonia. Mkazo ukiwa ni tafakuri ya
kujichambua kutoka kwa makanisa na watu binafsi, ili kutambua utu wa mwanadamu
na kuondoa mitazamo ya kibaguzi yenye fahamu na isiyo na fahamu na vizuizi vya
kimfumo ili kuhakikisha kwamba huduma ya diakonia inafanyakazi na kupatikana
kwa jamii nzima.
Mkazo huo
unaakisi kuwa, Makanisa ni ya uwazi, ya haki, ya ukarimu na yanajumuisha watu
wote, yakihakikisha kwamba jumuiya zilizo hatarini hazipuuzwi bali zinakuwa
wapokeaji wa huduma ya diakonia, kuelimisha jamii dhidi ya ubaguzi na kukuza
mazingira ambapo watu wanaohisi kubaguliwa kwa sababu ya rangi, jinsia, ulemavu
wanahakikishiwa usalama, heshima na wanapewa huduma wanazostahili.
“Wapendwa watu wa Mungu, ni imani yangu kuwa mtaombea Mkutano Mkuu huu na kushiriki katika siku ya ufunguzi.
“Ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye ametubariki kwa baraka zote za kiroho na kimwili (Efe 1:3-4),” alisema Askofu Malasusa.