NA GERALD LEONARD
BAADHI ya Wachungaji na Wainjilisti wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), wamesema kwa sasa maana halisi ya Kipaimara haipewi nafasi kama miaka ya nyuma, badala yake sherehe zimepewa umuhimu zaidi, hali ambayo inaweza kumtoa mtoto kwenye njia ya maadili na kumjua Mungu.
Kimsingi, Kipaimara katika KKKT ni hatua muhimu ya makuzi ya kiimani ambayo humwandaa mwamini kuelewa, kukiri, na kuishi imani ya Kikristo kwa ufahamu.
Licha ya baadhi ya Waksristo kuichukulia Kipaimara kama tukio la siku moja la kukiri imani hadharani, kiuhalisia ni safari ya mafundisho ya kina inayojengwa juu ya misingi minne: Biblia, Katekisimu ya Luther, Sakramenti, na maisha ya ufuasi wa Yesu.
Askofu mstaafu wa KKKT, Dayosisi ya Meru Dkt. Paul Akyoo, anasema maana halisi ya kipaimara ni watu kupata msingi wa mafundisho ya neno la Mungu ili kuimarisha imani yake na awe shahidi mwaminifu kwa mwokozi wake Yesu Kristo ili aweze kumshuhudia Yesu popote atakapokuwepo.
“Ni msingi wa mtu kuyashika mafundisho ya Neno la Mungu na kumshuhudia Yesu popote anapokuwepo kuwa ni shahidi mwaminifu wa huyu Yesu aliye mwokozi wa maisha yake, hayo mengine ni madogo sana, kikubwa ni msingi wa imani,” alisema.
Kauli yake inaungwa mkono na maandiko mbalimbali ya Kanisa la Kilutheri ambayo yanasema katika mafundisho ya Kipaimara, Biblia ndiyo dira ya kwanza na yanaweka mkazo kwamba mafunzo yote ya Kikristo hayawezi kusimama bila Neno la Mungu.
Katika muktadha huo, wanafunzi wa Kipaimara hujengewa msingi wa Biblia kutoka uumbaji, anguko la mwanadamu, hadi mpango wa ukombozi unaotimizwa na Yesu Kristo.
Katika torati na hasa kitabu cha Mwanzo, wanafunzi hujifunza asili ya mwanadamu na uhusiano wake na Mungu, wakati katika Injili hukutana na maisha ya Yesu, kifo chake na ufufuko wake na katika maandiko mengine ya Injili kama nyaraka za Mtume Paulo, hufundishwa dhana ya dhambi, neema, na haki kwa imani (Warumi 3, 5 na 6).
Uchambuzi wa msingi hapa ni kwamba Biblia haipewi tu kama kitabu cha historia ya wokovu, bali kama mwongozo wa maisha na wanafunzi hujifunza si tu “nini kilitokea,” bali “maana yake kwa maisha yao leo” jambo linalowafanya waone hitaji la Yesu Kristo na umuhimu wa kukua ndani ya imani.
Kuwabariki watoto
Ikumbukwe kuwa kila mwishoni mwa mwaka hasa ifikapo Novemba na Desemba, ni kipindi ambacho watoto waliohitimu mafundisho ya kiimani ya Kanisa ya miaka miwili, hubarikiwa na kuingia katika hali ya maisha mengine ya Mungu ikiwemo kushiriki meza ya Bwana.
Licha ya msingi wa mafundisho kuwa na lengo la kujenga wakristo wenye ufahamu, wenye tabia ya Kristo, na wanaoweza kushiriki ipasavyo katika maisha ya Kanisa, baadhi ya watumishi wanasema maana hiyo ni kama imewekwa kando.
Wanasema maana halisi ya Kipaimara ni ni kama imekuwa ikipotoshwa, kwani watoto wanapohitimu mafundisho na kubarikiwa, umuhimu huwekwa katika sherehe badala ya yale waliyofunishwa.
Mchungaji Anna Kuyonga wa KKKT, Dayosisi ya Mashariki na Pwani (DMP), Usharika wa Kijitonyama, anasema yeye hutamani kuona mtoto anapata kitu cha kiroho ndani ya moyo wake kutokana na mafundisho, kuliko kuweka kipaumbele kikubwa cha sherehe.
Alisema katika sherehe hizo utakuta watu wameweka vitu kama pombe, hali ambayo sio nzuri na kwamba kawaida sherehe ya kipaimara huwa inamuhusu mtoto, wazazi, wadhamini na watu wengine wachache.
“Sherehe siyo mbaya lakini ushauri wangu wasifanye kama ya harusi kwani, unaweza kufanya sherehe kubwa lakini ukakuta yale ambayo mtoto amefundishwa kanisani ameyaacha pale pale,” alisema.
Kauli yake inaungwa mkono na mwenzake wa KKKT, Kanisa Kuu Dayosisi ya Kaskazini Kati, Mchg. Paulo Metili ambaye anasema Kanisa linafanya kazi ya kufundisha watoto na kuwapa kipaimara lakini ni wazi kwamba kipaimara kimeingiliwa, kwani sherehe zimekuwa kubwa za kifahari na umakini usipokuwepo mtoto anaweza kutoka kwenye lile alilolipokea.
Mwinjilisti wa KKKT - DMP, Mtaa wa Kilakala, Laban Mnzava, anasema siku zilizopita kipaimara ilikuwa ni sherehe ndogo ya kifamilia, ikihusisha watumishi wa Kanisa ambao mara nyingi walifika nyumbani na watoto walishiriki kwa pamoja na furaha ikiwa na maudhui ya Kikanisa.
Mwnj. Mnzava alisema kwa sasa watumishi wa Mungu wanaogopa kuhudhuria kwenye hizo sherehe kwa sababu wanayokutana nayo ni aibu. “Utasikia ombea sherehe, chakula na vinywaji, si utaombea mpaka pombe, kwa hiyo ni aibu na fedheha kwa Kanisa,” alisisitiza na kuongeza:
“Juzi tu niliwaita wazee wa Kanisa wawafute watoto midomo kwa sababu walikuwa wamepaka lipstiki, Kanisani tunawalea nyumbani ni kuwatunza kitu ambacho kinatokea katika leo Kanisani ni utandawazi watu wanaiga mahali pengi,” alisema Mwnj. Mnzava.
Mafundisho
Kadhalika watumishi hao wamezungumzia kuathirika kwa ufundishaji wa madarasa ya kipaimara, kutokana na wazazi wengi kuwahimiza watoto zaidi katika elimu ya shule kuliko kipaimara, huku wakitumia hata siku zilizopangwa kwa ajili ya mafundisho kwenda kwenye masomo ya ziada (tuition).
Mchg. Stima Chakoma KKKT, Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Mtaa wa Ikwiriri anasema hali ya mahudhurio hafifu kwa baadhi ya watoto, ambayo inawapa wakati mgumu wa kuwafuatilia na kuwafundisha.
Mwinjilisti Neema Munisi wa KKKT, Mtaa wa Yongwe alisema mzazi anamwamsha mtoto mapema na kumwandaa kwenda shuleni na kuhakikisha hakosi hata mara moja, lakini kwenye kipaimra atakupigia simu akwambie mtoto anajiandaa na mtihani na yuko bize tuisheni hata siku za Jumamosi.
Naye Mchg. Kuyonga alisema anatamani kuona pale mtoto anapoandikisha kipaimara wazazi waone umuhimu wa mafunzo hayo kama wanavyokazania masomo yake ya ziada ya shule (twisheni).
“Tunatamani kuona mtoto ameenda Kanisani kwenye mafundisho akirudi mzazi achukue daftari lake aangalie amefanya nini, afuatilie zile kazi alizopewa Kanisani, kwa mfano ahakikishe katekisimu anaijua, amri kumi za Mungu, imani ya Kikristo aifahamu hata kwa vitendo, sakramenti ya ubatizo na meza ya Bwana,” alisema Mchg. Kuyonga.
Katekisimu Ndogo ya Martin Luther ni moja wa nguzo za mafundisho ya Kipaimara na iliandikwa kuwasaidia Wakristo kuelewa mafundisho magumu ya Biblia kwa lugha rahisi, ikiwa na vipengele vinne muhimu: Amri Kumi za Mungu, Imani ya Mitume, Sala ya Bwana, na Sakramenti.
Wachambuzi wa maandiko wanasema kupitia mafundisho ya Kipaimara, Amri Kumi haziwekwi kama kanuni ngumu za kufuata, bali kioo kinachoonyesha mapenzi ya Mungu na pia udhaifu wa mwanadamu.
Kadhalika mwanafunzi anatambua hitaji la neema ya Kristo na kujifunza maadili ya uhusiano na Mungu na uhusiano na jirani ambayo ni misingi miwili ya maisha ya Kikristo.
Baada ya kubarikiwa
Askofu Mstaafu Akyoo anasema, hatua ya Kanisa kuwabariki wakiwa watoto, kuna maana ya kulinda huu msingi ambao utamsaidia mtoto kutovurugwa na michanganyo ya maisha anapokwenda katika safari ya elimu ya msingi, sekondari na Chuo kikuu.
Hata hivyo baadhi ya watumishi wanazungumzia hofu ya vijana hao kupotea na kutoonekana kanisani baada ya kubarikiwa, wakitaka Kanisa kuweka mifumo ya ufuatiliaji.
Mchg. Chakoma anasema changamoto watoto wengi wanapata kipaimara lakini baada ya hapo wanapotea na kwamba Kanisa linapaswa kujikita zaidi katika kutoa huduma ya shuleni ili kutengeneza Wakristo kwa sababu muda mwingi watoto wako shule.
Anasema, hali hiyo anaona kama inachangiwa na wazazi lakini pia watumishi kwa sababu ya kutokuwapo kwa mkakati wa ufuatiliaji baada ya watoto hao kumaliza.
“Mimi binafsi wanapomaliza, kabla ya kubarikiwa ninakaa na wazazi ili kuwahimiza kuhusu watoto kuhudhuria Kanisani lakini pia nakuwa na daftari la mahudhurio ya kila mtoto anapokuja Kanisani baada ya Ibada anasaini kwamba yupo,” alisema Mchg. Chakoma.
Naye Mch. Metili ambaye pia ni Chaplain wa Shule ya Sekondari Peace House, inayomilikiwa na KKKT Dayosisi ya Kaskazini Kati, anasema, Kanisa linatakiwa kujipanga upya, liboreshe huduma shuleni ili kutengeneza vijana wanaomcha Mungu ambao kesho na kesho kutwa watakuja kuwa viongozi wa Kanisa na Taifa.
“Mimi ni Chaplain wa Shule ya Kanisa, nimefungua darasa la kipaimara na ukiangalia watoto wanapata kipaimara wakiwa wadogo hivyo wanahitaji malezi na huduma hiyo iimarishwe,” alisema.
Mwnj. Munisi wa Mtaa wa Yongwe anasema watoto wanapobarikiwa kuwaona Kanisani ni ngumu, hivyo kuna namna wazazi wanatakiwa kuona jinsi ya kusimamia watoto kwenye elimu ya Kikristo.
“Mimi huwa nina tabia ya kusema wageni wangu waliopata kipaimara simameni, hapo utakuta wamekuja watoto watano wakati waliopata kipaimara ni zaidi ya 40, tunafurahia wazazi wanaoelewa na kufuatilia watoto wao kuhusu masomo ya Kanisani,” anasema.
Mwenyekiti Vijana DMP
Mwenyekiti wa Vijana KKKT, Dayosisi ya Mashariki na Pwani, William Shechambo, anasema wanafunzi wa kipaimara wakisha barikiwa huingia moja kwa moja katika Umoja wa Vijana, hivyo ni muhimu kila mzazi amkumbushe mtoto kuwa safari ya Imani bado inaendelea.
“Wakitoka Darasa la Jumapili, wakishabarikiwa wanaingia Ibada za watu wazima, huku wanakutana na kaka zao na dada, wanaomtumikia Mungu kupitia Umoja wa Vijana. Hivyo tunawahitaji sana damu changa hawa, watupe mawazo mapya na mchango mpya wa kukuza Kanisa la Mungu,” anasema Shechambo.
Anaongeza kuwa, katika maandalizi ya kubarikiwa sherehe hazipaswi kupewa kipaumbele cha kwanza katika muda huo, bali wazazi wanapaswa kumuandaa mtoto kiakili na kiroho ili Ibada ya Kipaimara iwe na maana nzito katika historia ya maisha yake hata atakapokuwa mzee na kuwarithisha watoto wake.
Kipindi hiki cha Majilio, sharika na mitaa mingi ya Dayosisi za KKKT, iko kwenye utaratibu wa kufanya Ibada za Kipaimara, ambapo wanafunzi waliohitimu mafundhisho ya Kanisa, kupewa taji la kuwa Wakristo waliokomaa kiroho.







