NA WILLIAM SHECHAMBO
MIONGONI mwa wazee wenye hekima waliowahi
kutokea katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya
Mwanga, Cleopa David Msuya amefariki dunia, huku viongozi mbalimbali na Wana
KKKT wakieleza namna walivyokuwa wakimfahamu enzi za uhai wake.
Hayati Cleopa Msuya (94), aliyekuwa Makamu wa Rais wa kwanza na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, amefariki dunia Mei 7, 2025 Dar es Salaam na kifo chake kuthibitishwa
kwa umma na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, viongozi wa
Kanisa na serikali wametoa pole kwa familia na kueleza kwa hisia tofauti,
upekee wa Mzee Msuya, enzi za uhai wake katika utumishi wa uuma na Kanisa.
Askofu Mteule Mwanga
Askofu Mteule KKKT Mwanga, Dkt. Daniel Mono,
pamoja na kutoa pole kwa jumuiya ya Wilaya ya Mwanga na Kanisa kwa ujumla,
alisema wiki tatu zilizopita, alikutana na Mzee Msuya, Dar es Salaam ambapo
alimpongeza kwa kuaminiwa na Mungu kuiongoza Dayosisi ya Mwanga.
“Wiki tatu zilizopita, nilifika nyumbani kwake
Upanga, akanikaribisha na pamoja na umri wake mkubwa, ni mtu ambaye moyo wake
ulikuwa bado umelielekea Kanisa hivyo tulizungumza mambo mengi kuhusu Kanisa,
tukaahidiana kwamba tungeonana tena.
“Kimsingi Kanisa limepoteza mtu ambaye ni
muhimu, amekuwa na mchango mkubwa kwa ustawi wa Dayosisi ya Mwanga na Wilaya
hii ya Mwanga, kila kona ameacha alama nyingi zinazoeleweka na hata kitaifa
amefanya mengi makubwa,” alisema.
Mbunge wa Mwanga
Mbunge wa Jimbo la Mwanga, Joseph Tadayo,
akizungumza kutokea bungeni jijini Dodoma, alisema yeye ni mbunge wa tatu wa
Jimbo la Mwanga, ambapo wa kwanza ni Mzee Msuya, ambaye enzi za uhai wake
alikaa madarakani kwa miaka 20 na kuwaletea maendeleo makubwa kupitia umoja
aliouweka miongoni mwa wananchi wa Mwanga.
“Nitoe pole kwa Wana Mwanga na taifa kwa
ujumla, Mzee Msuya alikuwa kiongozi mwenye maono mapana na amejenga misingi
mikubwa katika jimbo letu ambayo inatufanya tuendelee kujenga mambo mengi
mazuri juu ya misingi hiyo,” alisema.
Mjumbe Mkutano Mkuu KKKT Mwanga
Mwenyekiti wa Vijana KKKT Dayosisi ya Mwanga,
ambaye pia ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Dayosisi hiyo, Julian Kagambo, alisema
vijana wa Mwanga hawatamsahau Mzee Msuya kwa uwekezaji alioufanya katika Sekta
ya Elimu wilayani humo.
“Mioyo ya vijana sio tu wa KKKT ambako alikuwa
akisali, bali hata walio wa imani nyingine itaendelea kumkumbuka Hayati Mzee
Msuya kwa namna alivyounganisha watu kupitia mkazo wake kwenye eneo la elimu,
hakuna na masihara hapo.
“Kwenye Kanisa, alikuwa nguzo muhimu sana hata
wakati ule tulipopata pigo la kufiwa na Askofu Chediel Sendoro, alituunganisha
wana KKKT Mwanga ili tuwe imara na kuharakisha mchakato wa kumpata Askofu
mwingine, alitutia moyo sana hadi siku ya mwisho ya uchaguzi wa kumpata Askofu
Mteule Mono,” alisema.
Taarifa ya Rais Samia
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, usiku wa Mei 7,
mwaka huu, alitangazia taifa kifo cha Cleopa David Msuya, aliyewahi kuwa Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Tanzania na Waziri Mkuu, kilichotokea Mei 7, 2025 majira
ya saa tatu asubuhi katika Hospitali ya Mzena, jijini Dar es Salaam.
“Kwa masikitiko makubwa natangaza kifo cha
Makamu wa kwanza wa Rais na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mzee Msuya kilichotokea leo Mei 7, 2025 saa tatu asubuhi katika Hospitali ya
Mzena Jijini Dar es salaam alipokuwa akipatiwa matibabu ya moyo.
“Mzee Msuya ameugua muda mrefu na amekuwa
akipatiwa matibabu ndani na nje ya nchi ikiwemo Hospitali ya JKCI, Mzena na
kule London Uingereza,” alibainisha Rais Samia katika taarifa yake kupitia
Televisheni ya Taifa (TBC).
Kufuatia kifo hicho, Rais Dkt. Samia aliagiza
kuwepo na siku saba za maombolezo, ambapo bendera ya taifa katika maeneo yote
itapepea nusu mlingoti na kuongeza kuwa taarifa zaidi kuhusu mazishi ya
kiongozi huyo zitatolewa na serikali.
Cleopa David Msuya ni Mtanzania pekee aliyewahi
kuteuliwa kwa kofia ya Waziri Mkuu na Marais wawili tofauti, akianza Baba
wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere na baadaye Rais wa awamu pili,
Ali Hassani Mwinyi.
Msuya ni nani?
Alizaliwa Januari 4, 1931 katika Kijiji cha
Chomvu, Usangi wilayani Mwanga, Mkoa wa Kilimanjaro na kushika nyadhifa
mbalimbali serikalini.
Kuanzia mwaka 1964, Msuya alihudumu kama Katibu
Mkuu katika wizara mbalimbali, ambazo ni Wizara ya Maendeleo ya Jamii na
Utamaduni (1964–1965), Wizara ya Ardhi, Makazi na Maendeleo ya Maji
(1965–1967), Wizara ya Mambo ya Uchumi na Mipango (1967–1970), na Wizara ya
Fedha (1970–1972).
Februari 18, 1972, aliteuliwa kuwa Waziri wa
Fedha na alihudumu hadi alipohamishiwa kuwa Waziri wa Viwanda mnamo tarehe 3
Novemba 1975. Baada ya kuhudumu kwa miaka mitano kama Waziri wa Viwanda,
aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu mnamo Novemba 1980, nafasi aliyoshikilia hadi
Februari 1983.
Baadaye alirudi tena kuwa Waziri wa Fedha
kutoka Februari 1983 hadi Novemba 1985.
Novemba 6, 1985, alipewa jukumu jipya akiwa
Waziri wa Fedha, Mambo ya Uchumi na Mipango hadi Machi 1989. Kisha alirudi kuwa
Waziri wa Fedha tena kuanzia Machi 1989 hadi Desemba 1990, na baadaye kuwa
Waziri wa Viwanda na Biashara kutoka Machi 1990 hadi Desemba 1994.
Mwaka 1994, aliteuliwa tena kuwa Waziri Mkuu
kwa mara ya pili, na pia kuhudumu kama Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania hadi Novemba 1995. Katika uchaguzi wa Bunge wa mwaka 1995,
alichaguliwa tena kuwa Mbunge na alihudumu hadi alipojitokeza kustaafu rasmi
tarehe 29 Oktoba 2000.
Baada ya kustaafu, Msuya aliendelea kuwa
mwanachama hai wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), na kufikia mwaka 2006 alikuwa bado
ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM. Pia alikuwa
Mwenyekiti wa Jukwaa la Maendeleo la Kilimanjaro.
Oktoba 23, 2019, akiwa na umri wa miaka 88, Cleopa Msuya aliteuliwa na Rais Hayati John Pombe Magufuli kuwa Mkuu wa Chuo ‘Chancellor’ wa Ardhi Institute (Chuo Kikuu cha Ardhi).
Bwana Ametoa, Bwana Ametwaa, Jina la Bwana Lihimidiwe!