MABINTI 8,000 WAKATISHWA MASOMO KWA MIMBA, NDOA ZA UTOTONI

Font size:

NA WILLIAM SHECHAMBO, Nachingwea

NI zaidi ya miongo mitatu sasa Tanzania imekuwa katika mjadala wa namna ya kudhibiti ndoa za utotoni ambazo bado zinashamiri katika baadhi ya mikoa, hususani maeneo ya vijijini.

Wakati mapambano hayo yakiendelea, Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 bado inatoa uhuru kwa msichana mwenye umri wa miaka 14 na mvulana mwenye miaka 18, kuolewa na kuoa. Sintofahamu inatokea.

Sheria hiyo inaleta mkanganyiko na kuwavuruga zaidi watu wa kawaida katika jamii, ambao wanahitaji kujitosa katika mapambano ya kukomesha ndoa za utotoni.

Wakati Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 inaeleza bayana kwamba mtoto ni mtu mwenye umri chini ya miaka 18, na kwa msingi huo kisheria mtoto hana maamuzi yake binafsi, sheria ya ndoa ya mwaka 1971 inafungua ‘uchochoro’ wa kuozesha watoto.

Ingawa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haitamki mahususi umri wa mtoto, mbali tu ya kutaja sifa za raia kuruhusiwa kupiga kura kuwa ni umri wa miaka 18, kwa maana hiyo inatoa mwelekeo kwamba umri wa mtu kujiamulia mambo yake mwenyewe ni miaka 18.

Kwa mantiki hiyo, sheria inayoruhusu msichana wa umri wa miaka 14 kuolewa inaonekana kukinzana kimantiki kuwa na umri mpevu wa mtu kufanya maamuzi yanayohusu maisha yake, ambao kisheria unatambuliwa kama miaka 18 kwa mujibu sheria ya mtoto ya mwaka 2009.

Sheria ya ndoa ilifanyiwa mabadiliko mwaka 2019 na yaligusa masuala ya kugawana mali baina ya wanandoa katika talaka, hata hivyo mabadiliko hayo hayakugusa kipengele cha umri wa msichana kuolewa, jambo ambalo linakoleza mjadala wa wadau wa sheria, watetezi wa haki za kijinsia na wanaharakati wa haki za binadamu kwa ujumla.

Baadhi ya wanaharakati wamewahi kupeleka shauri mahakamani kupinga umri wa msichana kuolewa kuomba mahakama ibatilishe umri huo, mahakama iliagiza serikali kufanya hivyo, hata hivyo hakuna mabadiliko yoyote yaliyofanyika mpaka sasa.

Mfano mzuri ni shauri la Rebeca Gyumi dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuhusu umri wa msichana kuolewa. Mahakama iliamua kuwa Serikali ichukue hatua ndani ya mwaka mmoja kubadilisha vifungu vya 13 na 17 vya Sheria ya ndoa ambavyo vilikuwa vinabagua kati ya mtoto wa kike na wa kiume kuingia katika ndoa. Vigungu hivyo vinataja umri wa msichana kuolewa kuwa ni miaka 15, wakati mvulana ni miaka 18.

Kimantiki, vifungu vya 13 na 17 vya Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 vinakinzana na sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009; Sheria ya Elimu ya mwaka 1978 na marekesbisho yake yote, mikataba mbalimbali kuhusu haki za watoto ambazo Tanzania imeridhia kama mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watoto (UNCRC) na hata Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kote huko umri wa mtoto unafafanuliwa kuwa ni chini ya miaka 18.

Kutokana na hali hiyo, Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), ambalo kwa takwimu za hivi karibuni lina waumini 8,500,000 na kulifanya kuwa la tatu duniani kwa madhehebu ya Lutherani nyuma ya Ujerumani na Ethiopia, limejitosa kusaidia juhudi za kukomesha ndoa za utotoni.

Kupitia mradi wake wa ‘Hakuna Marefu yasiyo na mwisho’, KKKT inatekeleza kwa vitendo wajibu wake wa kuwafundisha waumini habari za Kristo na ulimwengu ujao na maisha ya hapa duniani ambayo yanampendeza Mungu kwa kupinga vitendo vya unyanyasaji na ukatili wa kijinsia baina ya wanadamu.

Utafiti uliofanywa na shirika la Twaweza mwaka 2023 ulionyesha kwamba mkoa wa Lindi ni wa tano nchini kati ya mikoa yenye viwango vya juu vya ndoa za utotoni nchini ukiwa na asilimia na 48. Kinara wa ndoa hizi ni Shinyanga wenye asilimia 59, Tabora asilimia 58, Mara asilimia 55 na Dodoma asilimia 51.

Mkuu wa Mkoa

Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zeinab Telack, amesema kuwa kwa mwaka 2024 ndani ya mkoa huo, jumla ya watoto 7,840 wenye umri kati ya miaka 10 hadi 19, wamepata mimba na kukatisha masomo, jambo ambalo halikubaliki katika jamii na serikali kwa ujumla.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa, kati ya hao 7,840 wenye umri wa kati ya miaka 10-14 ni 93 na wenye umri wa miaka 15-19 ni 7,745.

Watuhumiwa walionaswa kuhusika na uhalifu huo, amesema wameshughulikiwa kwa mujibu wa sheria na wengine wanaendelea kutafutwa kwa utaratibu wa kawaida wa upelelezi katika wilaya zote za mkoa wa Lindi.

Mkuu wa Wilaya

Naye Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Mohamed Hassan Moyo, anasema katika wilaya hiyo vita dhidi ya ndoa za utotoni na mimba za utotoni inakwenda sambamba, na matokeo yake ni mazuri ikilinganishwa na hali ilivyokuwa awali.

Anasema maeneo ya katikati ya mji, ukatili wa kijinsia unaosababisha ndoa za utotoni unaendelea kutoweka, hivyo nguvu kubwa inaelekezwa katika elimu kwa umma unaoishi kwenye kata zilizo pembezoni ambazo zinaonekana kuwa za vijijini.

Anasema hatua iliyofanyika ni kutoa elimu endelevu kwa jamii kuthamini elimu, kutumia nyumba za dini kutangaza umuhimu wa malezi bora ya watoto na kufuatilia kwa ukaribu mwenendo wa wanafunzi wanaofaulu elimu ya sekondari na idadi sahihi wanaokwenda shuleni.

“Mimba za utotoni bado zipo na hii inatokea kwa wale wasichana wachache wanaojihusisha na vitendo vya ngono wakiwa bado wadogo,” anasema.

Moyo anasema, wanaendelea kukusanya taarifa kwa kushirikiana na wenyeviti wa serikali za mitaa, kujua hali halisi ya sasa baada ya kazi kubwa iliyofanyika na vitengo mbalimbali vya serikali na wadau.

Maendeleo ya Jamii

Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea, Stella Kategile, akizungumza na gazeti la Upendo amesema wamefanikiwa kutoa elimu kwa jamii, wakiwamo wazazi na wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.

“Hapa Nachingwea tumeanzisha mpango unaitwa ‘Shule Salama’, ambao una kazi kubwa ya kutoa elimu ya kupambana na ndoa za utotoni na mimba za utotoni, tangu tuianze imekuwa na manufaa makubwa,” anasema.

Akitoa takwimu anasema kwa muda mfupi tangu kuanza kwa mpango huo, katika miaka mitatu iliyopita hadi mwaka huu Februari, wamefanikiwa kuwaokoa mabinti 34 kutoka katika mazingira ambayo yalikuwa na viashiria vya kuozeshwa wakiwa bado na umri mdogo.

“Watoto hawa tumewaokoa na kuwatafutia ada na vifaa vyote vinavyohitajika, hivi ninavyozungumza nawe, wapo shuleni mikoa mbalimbali wanasoma, lakini walikuwa tayari kwenye mipango ya kupewa waume ili waanzishe familia zao,” anasema.

Mwenyekiti wa Kijiji

Mwenyekiti wa Kijiji cha Nambambo, Rehema Kampela, anasema Kijiji chake ni miongoni mwa vijiji ambavyo vimefanikiwa kupambana na mila potofu za kuwaozesha wasichana wakiwa bado wadogo.

Alisema kwa miaka ya nyuma, kulikuwa na utamaduni huo, lakini sasa baada ya kujengwa kwa shule ya kisasa ya Sekondari Nambambo, iliyojengwa kwa fedha za UVIKO-19, Watoto wakimaliza shule ya msingi wanaendelea na masomo.

“Umbali wa shule, elimu duni kwa wazazi na walezi viliturudisha nyuma katika hili suala unalolisema, lakini sasa tunashukuru watu wanaelimika wanajua umuhimu wa elimu kwa watoto wao,” alisema. 

Jeshi la Polisi

Takwimu za Jeshi la Polisi Nachingwea zinaonyesha kupungua kwa mashauri ya ukatili wa kijinsia. Mathalani, matukio yanayowafikia yanahusu mabinti wadogo walioolewa ni kutoka mikoa mingine na jamii za wafugaji wanaoingia Nachingwea kwa malisho.

“Kwa Nachingwea, jamii ya hapa wamebadilika sana, suala la ndoa za utotoni lipo kwa wahamiaji tena wale wanaoingia kimagendo bila kutoa taarifa kwa serikali za mitaa.

"Wengi wa hawa si wakazi wa Nachingwea na wanaishi porini sana kwa kuhamahama, hivyo binti mdogo akipata upenyo wa kukimbia madhila ya ile ndoa anatokea kwa jamii na kusaidiwa kufika kwetu," alisema Mkuu wa Dawati la Jinsia Nachingwea, Asha Mponda.

Alisema hivi karibuni, walifanikiwa kuwarejesha mabinti watatu makwao baada ya kufanikiwa kutoroka kwa watu wazima waliowaoa na kuanza kuzunguka nao na mifugo, harakati za kuwatafuta zinaendelea licha ya kwamba ni jamii za wanaohamahama na mifugo.

Wananchi

Wanawake wa Nachingwea waliozungumza na gazeti hili katika Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani mwaka huu wa 2025, wamesema bado kuna kazi kubwa katika vita dhidi ya ndoa za utotoni kwani jamii zinaficha taarifa za matukio hayo.

Violet Mkisi mkazi wa Nachingwea Mjini, anasema amehamia Nachingwea kikazi, lakini haoni kama kweli matukio ya ndoa za utotoni yamekwisha bali usiri wa familia umesababisha utulivu wakihofia mkono wa sheria.

Mkazi mwingine wa Nachingwea Mjini, Tabu Migomba, anasema wenyeviti wa vijiji na serikali za mitaa, wanatakiwa kuwa mstari wa mbele kuhakikisha matukio ya ndoa za utotoni yanaripotiwa na wahusika wanakamatwa.

“Sasa hivi na uwepo wa Mama yetu Rais Samia Suluhu madarakani, wanawake hatutaki mchezo na mabinti zetu, ndoto za wasichana wadogo lazima zitimie na yeyote anayecheza na mabinti kwa kuwakatisha masomo ni wajibu wa viongozi kule chini yaani wenyeviti wa mitaa kupambana nao,” anasema. 

Ni wazi kuwa jitihada kwa ngazi ya chini zinafanyika wilayani Nachingwea, hivyo ni wakati sasa serikali kutafuta suluhu ya kudumu ya kisheria, ikiwemo kupeleka muswada wa mabadiliko ya sheria ya ndoa bungeni, ili kubadili kifungu cha umri sahihi wa msichana kuolewa kutoka umri wa miaka 14 hadi 18 ili kuendana na tafsiri ya umri wa mtoto.

Kufanya hivyo kutasaidia kupunguza tatizo la ndoa za utotoni, kumuinua msichana kielimu kwa kuwa itawapa muda wa kusoma badala ya kuozeshwa katika umri mdogo.

ends

or

For faster login or register use your social account.

Connect with Facebook