ASKOFU MALASUSA, TEC, CCT, BAKWATA WALAANI KUSHAMBULIWA DKT. KITIMA

Font size:

MKUU wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dkt. Alex Gehaz Malasusa, amesema Kanisa limeshtushwa, kusikitishwa na kuumizwa kwa tukio la kushambuliwa na kujeruhiwa kwa Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Dkt. Charles Kitima.

Padri Charles Kitima alivamiwa na watu wawili na kujeruhiwa Aprili 30 mwaka huu, majira ya saa 4 usiku katika makazi na Makao Makuu ya TEC, Kurasini - Dar es Salaam,  na sasa anaendelea na matibabu hospitali ya Aga Khan, Dar es salaam.

Taarifa ya Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam ya iliyotolewa Mei 1, 2025, ilieleza kuwa mtu mmoja anashikiliwa kwa tuhuma za kuhusika na shambulio hilo dhidi ya Padri Kitima.

Kwa mujibu wa mashuhuda waliokuwepo katika mgahawa mmoja ndani ya viunga vya TEC, Padri Kitima alionekana akiwa katika mazungumzo na baadhi ya watu kabla ya kuinuka kuelekea msalani.

Dakika chache baadaye, watu wasiojulikana walitokea ghafla na kumshambulia kwa muda mfupi kisha kutoweka mara moja.

Baada ya tukio hilo, Padri Kitima alikutwa akivuja damu sehemu mbalimbali za mwili na kuomba msaada na kupewa huduma ya kwanza katika kituo kidogo cha afya kilichopo ndani ya eneo hilo, kabla ya kusaidiwa kupandishwa kwenye gari na kupelekwa hospitalini kwa matibabu zaidi.

Kutokana na tukio hilo, Askofu Dkt. Malasusa amesema, jambo la kusikitisha ni kuona taifa linaendelea kushuhudia matukio ya kinyama yasiyostahili wanadamu wenye utu kuyafanya dhidi ya mwanadamu mwingine.

“Kumvizia mtumishi wa Mungu kumetuumiza, si tu kwa ajili ni mtumishi wa Mungu lakini tunaona matukio haya yamevuka mipaka, ule woga na heshima imepungua sana katika taifa,” alisema Askofu Dkt. Malasusa akizungumza na Upendo Media.

Vilevile, alitumia nafasi hiyo kuwataka Wakristo na waumini wa madhehebu na dini zingine kuliombea taifa ili uovu kama huo usiendelee, huku akimtakia Dkt. Kitima afya njema na kupona kwa haraka.

 

TEC

Makamu wa Rais wa TEC, Askofu Eusebius Nzigilwa, katika tamko la baraza hilo, naye kwa niaba ya baraza hilo, alieleza kusikitishwa na kulaani kitendo cha kushambuliwa na kujeruhi kwa Dkt. Kitima na kukiita kuwa ni kitendo kiovu.

“Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) limesikitishwa sana na linalaani tukio baya la uovu la kuvamiwa, na kujeruhiwa kwa Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Tanzania,” imeeleza taarifa ya Askofu Nzigilwa.

Katika taarifa hiyo, TEC imetoa rai kwa Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya usalama kuchukua hatua za haraka za kuwabaini na kuwakamata wote waliohusika katika kupanga na kutekeleza uhalifu huo wa kinyama na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.

 

CCT

Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), katika kueleza masikitiko yake kuhusu tukio hilo, imeeleza kuwa imepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa na inalaani vikali shambulio hilo dhidi Padri Dkt. Kitima.

Mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Askofu Dkt. Fredrick Shoo, alisema katika taarifa rasmi ya CCT kuwa, wanatoa pole kwa Rais wa Baraza, Maaskofu, Mapadri, Watawa, Waumini na Watanzania wote wenye mapenzi mema kwa mahangaiko waliyoyapata mara tu baada ya taarifa ya tukio hilo la kinyama.

“Kipekee uongozi na Jumuiya ya Kikristo Tanzania tunapenda kutoa pole sana kwa Padri Kitima ambaye alipata maumivu ya moja kwa moja kutokana na tukio hilo na tunamuombea uponyaji wa haraka.

“Jumuiya inaitaka Serikali na vyombo vya dola kwa ujumla kuhakikisha waliojihusisha na tukio hili baya wanapatikana na vitendo kama hivi vinakemewa vikali na vinakomeshwa ili kutokutokea tena.

“Hivi karibuni tumeanza kusikia na kushuhudia vitendo kama hivi maeneo mbalimbali, sasa ni wakati muafaka wa kuhakikisha kuwa vitendo hivi vinazuiliwa kwani vinaleta taswira hasi kwa Taifa pamoja na maumivu makubwa kwa wahusika na jamii kwa ujumla,” alisema Askofu Dkt. Shoo.

 

BAKWATA

Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Alhaj Nuhu Jabir Mruma, alisema baraza hilo, linalaani vikali tukio hilo lililotokea Jumatano wiki hii la kushambuliwa kwa Dkt. Kitima.

Kwa mujibu wa taarifa maalumu aliyoitoa Alhamisi wiki hii, Alhaj Mruma alivitaka vyombo vinavyohusika kufanya uchunguzi wa kina na haraka na kuwachukulia hatua watakaobainika kufanya shambulio hilo.

Katika taarifa hiyo, Alhaj Mruma alitoa rai kwa Waislamu na Watanzania kwa ujumla, kuendelea kuwa na subira wakati vyombo vikiendelea na uchunguzi.

Alhaj Mruma alisema BAKWATA na Mufti kwa ujumla, wanamtaka kila Mtanzania popote alipo, kuwa balozi wa amani na kuendelea kuilinda amani na utulivu wa nchi, amani ambayo ni tunu ya taifa la Tanzania.

Padri Dkt. Kitima ni mmoja wa viongozi mashuhuri wa Kanisa Katoliki nchini, ambaye amekuwa mstari wa mbele katika kupaza sauti dhidi ya ukandamizaji wa haki, ukiukwaji wa sheria na katika kupigania demokrasia na haki za binadamu.

or

For faster login or register use your social account.

Connect with Facebook