Taasisi ya Wisevoter ya nchini Marekani, inayohusika na ufanyaji wa utafiti kuhusu masuala mbalimbali, imezitaja nchi tano za Afrika zinazoongoza kwa wanandoa kuachana kwa talaka.
Katika orodha hiyo, Libya inaongoza ikifuatiwa na Misri, Mauritius, Algeria, visiwa vya Shelisheli (Seychelles) na Sudan.
Utafiti huo uliofanyika mwaka 2020, unaeleza kuwa pamoja na kuwa talaka ni utaratibu au mchakato wa kisheria unaoruhusu mume na mke kuachana na kuvunja ndoa yao, lakini katika nchi hiyo hali hiyo inatisha.
Matokeo ya utafiti huo yameungwa mkono na watafiti wengine wawili, akiwemo Sherley Clack ma Sarah Otto, ambao wametafiti na kubaini kuwa nchi ya Afrika Kusini nayo inakuja kwa kasi katika kundi hilo.
Mwanasheria wa kujitegemea hapa Dar es Salaam, Samuel Thomas, anasema taratibu za talaka zinaweza kutofautiana kati ya nchi na nchi, dini na dini na zinaweza kusimamiwa na sheria za kidini, sheria za kiraia au kitamaduni.
"Kuvunjika kwa familia ni jambo la kawaida sehemu zote duniani, ikiwa ni pamoja na Afrika, lakini bara hili mara nyingi hupongezwa kwa kuwa na uhusiano imara wa kifamilia," anasema.
Hata hivi, anasema kwa utafiti kadhaa, miaka ya hivi karibuni inabadilisha uhalisia na kwa sasa Afrika inapitia mabadiliko katika maisha ya ndoa ambayo yamesababishwa na mambo mbalimbali ikiwemo utandawazi.