BoT KUWABANA WAKOPESHAJI FEDHA KIHOLELA

Font size:

Benki Kuu ya Tanzania (BoT), imesema kwa mujibu wa Kifungu cha 16(1) cha Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018, ni kosa kwa taasisi, kampuni au mtu binafsi kujihusisha na biashara ya kutoa mikopo bila ya kuwa na leseni.

Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba, amesema kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari kuwa, BoT haitasita kuwachukulia hatua za kisheria, taasisi, kampuni au watu binafsi wanaofanya biashara ya kukopesha fedha kiholela.


"... Kwa mujibu wa kifungu cha 16(2)(a) cha Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2018, hatua zitakazochukuliwa kwa ukiukaji wa Sheria ni pamoja na faini isiyopungua Shilingi Milioni 20 au kifungo cha muda usiopungua miaka miwili au vyote viwili kwa pamoja," amesema Gavana Tutuba kupitia taarifa hiyo.

Kadhalika amesema Benki Kuu inawakumbusha wakopaji wote kuhakikisha wanasoma mikataba ya mikopo inayotolewa na wakopeshaji, kuelewa na kukubaliana na vigezo na masharti ikiwa ni pamoja na riba na gharama nyingine za mikopo hiyo.

Gavana amesisitiza kuwa, mkopeshaji anatakiwa kutoa nakala ya mkataba wa mkopo kwa mkopaji, kadhalika mkopaji ana haki ya kudai na kupewa mkataba wa mkopo kila anapochukua mkopo.

"Tunapenda kuusisitizia umma kuepuka kukopa au kufanya biashara na taasisi, kampuni au mtu binafsi ambae hana leseni kutoka Benki Kuu.

"Orodha ya taasisi, kampuni na watu binafsi wenye leseni za biashara ya kukopesha zinatolewa na Benki Kuu ya Tanzania kwenye tovuti yetu ambayo ni www.bot.go.tz," ameeleza Gavana Tutuba.


or

For faster login or register use your social account.

Connect with Facebook