Wanamgambo wenye silaha wamewaua zaidi ya raia 35 na kuwajeruhi wengine kadhaa, katika shambulio lililotokea usiku wa Jumatatu, wiki hii katika vijiji baadhi vya jimbo la Ituri Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.
Kiongozi wa kundi la Djaiba katika vijiji vya Djugu JEAN VIANNEY amesema wanamgambo wa CODECO wametekeleza shambulizi hilo ambalo lilianza majira ya saa mbili usiku, wakiwauwa wakaazi kwa kuwapiga risasi na kuziteketeza nyumba zao kwa moto.
Pia ameongeza kuwa, wapo watu waliojeruhiwa na wengi wamepoteza maisha kutokana na kuungua na moto ndani ya nyumba zao.
Kiongozi wa asasi za kiraia katika eneo hilo JULES TSUBA amesema miili 49 imepatikana hadi kufikia asubuhi ya leo, Februari 2, 2025 wakati ambapo bado juhudi za kutafuta waathirika zaidi zikiendelea kuchukuliwa.
CODECO ni moja ya makundi mengi ya wanamgambo yanayopigania ardhi na rasilimali mashariki mwa DRC.