Maaskofu wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) na wenzao wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), wanakutana kwa siku mbili Dar es Salaam chini ya mwamvuli wa Tume ya Kikristo ya Huduma za Jamii (CSSC).
Kusanyiko hilo linajumuisha Maaskofu zaidi ya 100, ambapo ajenda mojawapo ni kujadili utoaji wa huduma endelevu za Afya na Elimu kwa sasa na miaka ijayo, ili kuweka mikakati bora zaidi ya kukabiliana na changamoto mbalimbali.
Akifungua Mkutano huo Rais wa CSSC, Askofu wa KKKT - Dayosisi ya Kaskazini Dkt. Fredrick Shoo, amesema pamoja na mafanikio makubwa yaliyopo kupitia huduma hizo, bado kuna changamoto nyingi zinazotokana na mabadiliko ya mifumo, sera za nchi, sheria na uwepo wa mila na desturi zinazosababisha wanawake kuendelea kujifungulia nyumbani.
Baadhi ya Maaskofu walioshiriki mkutano huo akiwemo Mkuu wa Kanisa la Mennonite Tanzania, Askofu Nelson Kisare, wamesema huduma za Jamii zinazotolewa na Kanisa, ni sehemu muhimu ya kuendelea kuhubiri Injili ya kweli kwa watu huku wakisisitiza umuhimu wa kujipanga vizuri kukabiliana na changamoto zote zinazojitokeza.
Katibu Mkuu wa CSSC, Padre Charles Kitima amesema pamoja na Kanisa kufanya vizuri katika masuala mengi, suala la kukemea dhambi katika jamii lipewe mkazo.
Tangu kuanzishwa kwa CSSC miaka 33 iliyopita, tume hiyo imesaidia kuwepo kwa zaidi ya taasisi 1,000 za elimu na afya zinazotoa huduma kwa usawa bila ubaguzi.