Baraza la Madiwani Jiji la Mbeya wameridhia ombi la kuligawa Jimbo la Mbeya mjini na kupata majimbo mawili ili kuongeza kasi ya maendeleo kwa Wananchi katika jiji hilo.
Uamuzi huo umefikiwa leo, Machi 12, 2025 katika Kikao cha Baraza la Madiwani, ambacho kimeketi pamoja na mambo mengine kujadili hoja ya kuridhia jimbo hilo kugawanywa.
Timu ya Menejimenti imependekeza Jimbo la Mbeya mjini libaki na kata 23 na mitaa 121 na kuwa na Jimbo jipya pendekezwa la Uyole libaki na Kata 13 na mitaa 60.
Wakizungumza baada ya kikao hicho, Madiwani kutoka katika kata mbalimbali za jiji la Mbeya, wameeleza kuwa ugawaji wa jimbo hilo utakuwa na manufaa kwa wana Mbeya.
Jimbo hilo kwa sasa linaongozwa na Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson Mwansasu.