Bei ya mafuta ya petroli na dezeli imeendelea kuongezeka kwa miezi miwili mfululizo huku kwa watumiaji wa petroli wakilazimika kuzama zaidi mfukoni.
Taarifa hiyo imetolewa leo Jumatano Aprili 2, 2025 na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Dkt. James Andilile.
Bei ya mafuta ya PetroIi, Aprili hii kwa mafuta yanayopitia bandari ya Dar es Salaam yatauzwa sh. 3,037 kwa lita moja ambayo imeongezeka kutoka sh. 2,996 Machi, huku dizeli ikipaa kutoka sh. 2,885 Machi hadi sh. 2,936 mwezi huu.
EWURA imeeleza kuwa, kwa mafuta yatakayopitia Bandari ya Tanga, petroli itauzwa sh. 3,083 ikitoka sh. 3,042 Machi na dizeli ikipaa kutoka sh. 2,932 Machi hadi sh. 2,982.
Petroli itakayopita katika bandari ya Mtwara, lita moja itauzwa kwa sh. 3,109 ikilinganishwa na sh. 3,069 mwezi uliopita, huku dizeli ikiuzwa sh. 3,008 mwezi huu ikilinganishwa na sh. 2,958 ya Machi.